Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Hawza, mfululizo wa masomo ya Mahdawiyyah kwa anuani isemayo “Kuielekea Jamii Bora” unaolenga kueneza mafundisho na elimu zinazohusiana na Imam Mahdi (aj) umeandaliwa kwa ajili ya wasomi na wapenzi wa elimu. Baadhi ya Aya zinazomhusu Hadhrat Mahdi (aj) na mapinduzi yake ya kimataifa ni kama ifuatavyo:
Aya ya Kwanza:
«وَلقَدْ کَتَبْنا فِی الزّبُورِ مِنْ بَعْدِ الذّکْرِ أنّ الارضَ یرِثُها عِبادِیَ الصّالِحُونَ»
“Hakika tulikwishaandika katika Zaburi baada ya Ukumbusho kuwa: ardhi hii itarithiwa na waja wangu wema.
” (Al-Anbiya (21): 105)
Aya hii inazungumzia moja ya thawabu dhahiri za kidunia za watu wema – yaani utawala juu ya ardhi. Katika baadhi ya riwaya tukio hili muhimu limefasiriwa kuwa litatokea katika zama za kudhihiri Hadhrat Mahdi (aj).
Maana ya Maneno ya Aya:
«Zabur» ya Daud (au kwa mujibu wa vitabu vya Agano la Kale, Mazamir (Zaburi) za Daud) ni mkusanyiko wa dua, nyiradi na nasaha za Nabii Daud (as).
«Dhikr» kimsingi humaanisha kitu kinacholeta ukumbusho, lakini katika aya hii – kutokana na kufasiriwa kabla ya Zaburi – imetajwa kumaanisha Taurati, kitabu cha mbinguni cha Nabii Musa (as).
«Ardhi» humaanisha dunia yote isipokuwa panapokuwa na dalili mahsusi kinyume chake.
«Irthi» humaanisha kitu kinachohamishiwa kwa mtu bila muamala wa biashara. Katika Qur’ani Tukufu, neno hili mara nyingine hutumika kumaanisha ushindi wa watu wema juu ya watu waovu na kumiliki neema na rasilimali zao. (Tazama: Al-A‘raf (7): 137)
Kwa kuzingatia kwamba neno “waja” limeongezwa kwa “Mungu”, inaonyesha wazi imani na tauhidi yao. Na kwa neno “salihun” (صالحون), akili hukumbuka kila sifa njema: matendo mema na uchaji Mungu, elimu na maarifa, nguvu na uwezo, mipango bora, nidhamu na uelewa wa kijamii.
Wakati waja wa Mungu wenye imani watajipatia sifa hizi, Mwenyezi Mungu atawasaidia kuwashinda wenye jeuri.
Hivyo basi, “kudhoofishwa” pekee si sababu ya ushindi na utawala juu ya ardhi, bali imani na ustahiki ni nguzo kuu. Walionyongeshwa duniani hawatautawala ulimwengu mpaka watakapouhuisha misingi hii miwili.
Nukta Muhimu
1. Aali Muhammad (saww)
Kuhusiana na tafsiri ya aya hii, Imamu al-Baqir (as) amesema:
«هُمْ آلُ مُحَمَّدٍ یَبْعَثُ اللَّهُ مَهْدِیهُمْ بَعْدَ جَهْدِهِمْ فَیعِزُّهُمْ وَ یذِلُّ عَدُوَّهُمْ»
“Waja hawa wema ni Aali Muhammad; Mwenyezi Mungu atamleta Mahdi wao baada ya juhudi zao, kisha atawapa izza na atawadhalilisha maadui zao.”
(Kitabu al-Ghaybah, Shaykh Tusi, uk. 184)
Ni wazi kuwa maana ya hadithi hii si kwamba aya inawahusu wao pekee, bali inawataja kama mfano bora zaidi. Kwa hivyo, katika kila zama na kila mahali ambapo waja wema wa Mungu watainuka, watapata ushindi na hatimaye kuwa warithi duniani na utawala wake.
2. Bishara ya Utawala wa Walio wema katika Zaburi za Daud (as)
Katika Zaburi za Daud, maneno yanayofanana na yaliyomo katika Qur’ani yanaonekana mara kadhaa, jambo linaloonesha kuwa pamoja na upotoshaji mwingi uliotokea kwenye vitabu hivyo, sehemu hii imebaki salama.
“Wabaya wataangamizwa, bali wamtegemeao Mwenyezi Mungu watairithi dunia; muda mfupi tu na mwovu hataonekana tena; hata ukichunguza mahali pake, hautamwona.”
(Zaburi 37:9)“Lakini wanyenyekevu watairithi dunia, na watafurahia amani tele.”
(Zaburi 37:11)“Waliobarikiwa na Mwenyezi Mungu watairithi dunia, lakini waliolaaniwa naye wataangamizwa.”
(Zaburi 37:27)“Wenye haki watairithi dunia, na watakaa humo milele.”
(Zaburi 37:29)“Mwenyezi Mungu anajua siku za wema, na urithi wao utakuwa wa milele.”
(Zaburi 37:18)
Maneno haya yanaendana kabisa na maneno ya Qur’ani “عبادی الصالحون”. Vilevile, istilahi kama wema, waadilifu, wanyenyekevu, waliobarikiwa, na wanaomtumainia Mungu zinatajwa, zikionesha kuwa utawala wa watu wema ni wa jumla na unalingana na hadithi kuhusu kudhihiri kwa Hadhrat Mahdi (aj).
3. Utawala wa watu wema ni moja miongoni mwa sheria ya uumbaji
Ni lazima tufahamu kuwa tawala zote dhalimu ziko kinyume na mwelekeo wa uumbaji na kanuni za ulimwengu. Utawala unaokubaliana na asili ya uumbaji ni ule wa watu wema wenye imani. Mfumo wa maumbile ni ushahidi ulio wazi juu ya kukubalika kwa mfumo sahihi wa kijamii katika siku zijazo — jambo linaloelezwa wazi katika aya hii na hadithi zinazohusiana kuibuka Mkombozi Mkuu wa ulimwengu.
(Tafsiri ya Nemuneh, juzuu ya 13, uk. 515–524)
Utafiti huu unaendelea...
Imenukuliwa kutoka katika kitabu kiitwacho “Darsnameh Mahdawiyyat” kilichoandikwa na Khudamrad Salimiyan, huku ikifanyiwa mabadiliko kiasi.
Maoni yako